• October 7, 2025

Mafunzo ya Usalama wa Chakula – Ruben Centre

 

Mafunzo ya siku tatu yanayolenga wafanyabiashara wa chakula na akina mama kuhusu usalama wa chakula yameanza leo katika kituo cha Ruben Centre, jijini Nairobi. Kupitia programu hii, washiriki wanahimizwa kuzingatia ubora na usafi wa vyakula wanavyonunua sokoni, njia sahihi za kupika pamoja na mbinu za kuhifadhi chakula ili kuepuka magonjwa yanayowakumba mara kwa mara katika mitaa ya mabanda.

Akina mama pia wanapewa mwongozo wa namna bora ya kuwalisha watoto wao ili kuzuia utapiamlo, tatizo ambalo limekuwa changamoto kubwa katika familia nyingi kutokana na hali ngumu ya maisha. Wameelezwa kuwa lishe bora na chakula salama ni kinga dhidi ya magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kuhara ambayo mara nyingi huibuka katika maeneo yenye msongamano mkubwa.

Afisa wa Afya ya Umma wa Kaunti ya Nairobi, Bw. Orwa, ameitaka jamii kuhakikisha familia na wananchi kwa jumla wanapata chakula salama, akisema kila mmoja ana jukumu la kulinda afya yake na ya wenzake.

Kwa siku mbili zijazo, washiriki wanatarajiwa kuendelea kujifunza mbinu zaidi, hatua inayotarajiwa kuimarisha afya ya familia na kupunguza hatari ya milipuko ya magonjwa katika jamii ya Mukuru.

Read Previous

Illegal Abortions In Mukuru

Read Next

Usafi soko la Reli Mukuru kwa Ruben

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Most Popular