FALSE: Photo does not show the drought situation in Embolioi, Kajiado County, in October 2022
Wafanyabiashara katika eneo la Reli Mukuru jijini Nairobi wanalalamikia hali duni ya usafi inayoshuhudiwa sokoni, hali inayochangiwa na taka zinazotupwa ovyo pamoja na ukosefu wa vyoo vya umma. Wanasema hali hii imekuwa tishio kubwa kwa afya zao na afya ya wateja wanaotembelea soko hilo kila siku.
Wakizungumza na Ruben fm, baadhi ya wafanyabiashara wamesema licha ya wao kulipa ushuru wa kaunti mara kwa mara, huduma za usafi katika eneo hilo hazijaboreshwa. Wanadai suluhu ya kudumu ni kuwekwa kwa eneo maalum la kutupia taka, ambapo taka hizo zitakusanywa na kuondolewa mara kwa mara, pamoja na kujengwa vyoo vya umma vitakavyotumiwa na wakazi na wateja wa soko hilo.
Aidha, wamekwazika kwa nini kikosi cha NYS kimekuwa kikipelekwa mara kwa mara katika maeneo mengine kusafisha mitaa lakini hakijawahi kufika katika soko la Reli, licha ya changamoto kubwa za kiafya zinazotokana na uchafu huo. Wameeleza kuwa hali hiyo inawaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara.
Kwa sasa, wakazi hao wanasema wanasubiri majibu na hatua madhubuti kutoka kwa serikali ya kaunti pamoja na idara husika ili kuhakikisha mazingira safi na huduma muhimu za vyoo vya umma zinapatikana. Swali linalobaki ni, ni lini mamlaka husika yatawajali wananchi hawa na kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kulinda afya za wananchi wake?
Report by Alice Odera