• August 28, 2026

Daraja la Kuunganisha Kwa Reuben na Kwa Njenga Lapokelewa kwa Furaha

Ujenzi wa daraja la kuwavusha wananchi kati ya maeneo ya Mukuru Kwa Reuben na Kwa Njenga umepokelewa kwa furaha na afueni kubwa na wakazi wa maeneo hayo.

Kwa muda mrefu, wakazi waliokuwa wakitumia njia hiyo, hususan eneo la Kwa Reli, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za usalama, huku visa vya wizi, uporaji na baadhi ya watu kudungwa visu vikishuhudiwa katika eneo hilo.

Wakazi wanasema daraja hilo litasaidia kurahisisha usafiri na kupunguza hatari wanazokumbana nazo wakati wa kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine.

Baadhi ya wakazi wameeleza furaha yao, wakisema kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri kuona maendeleo katika eneo hilo. Wanatumai kuwa ujenzi wa daraja hilo hautaongeza tu usalama, bali pia utarahisisha shughuli zao za kila siku, hasa kwa wafanyabiashara, wanafunzi na wafanyakazi wanaotumia njia hiyo.

Hatua hiyo pia inatajwa na wakazi kuwa ni sehemu ya matokeo ya uangalizi na ufuatiliaji wa masuala ya jamii kupitia Ruben FM, ambayo imekuwa ikiangazia changamoto zinazowakabili wakazi wa Mukuru na kuzipa majukwaa ya kusikika na wahusika mbalimbali.

Hata hivyo, wakazi wanatoa wito kwa wahusika kuhakikisha kuwa daraja hilo linakamilishwa kwa viwango vinavyofaa na kuwekwa miundombinu ya kutosha ya usalama na taa, ili liwe salama kwa matumizi ya wananchi wakati wa mchana na usiku.

Kwa wakazi wa Kwa Reuben na Kwa Njenga, daraja hili ni zaidi ya njia ya kuvuka ni hatua muhimu ya kuunganisha jamii na kuboresha usalama pamoja na maisha ya wananchi.

report by: Robert Botere

Read Previous

Grief in Mukuru as Body of Two-Year-Old Boy Found in Ngong River

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Most Popular